Nyamato Mkuranga Site

Washiriki wa kanisa la Makongo Juu walikwenda Nyamato, wilayani Mkuranga, mkoa wa Pwani, pale wito wa kuyafikia maeneo mapya ulipotolewa mwaka 2004/5 na kuanzisha kanisa huko.

Baada ya mafanikio haya, kwa neema ya Mungu, kiwanja kilitafutwa na kuandaa sehemu ya ibada.Sehemu hii ilikuwa kwa ajili ya kuwapa washiriki kivuli kujiepusha na jua kali na mvua, na si zaidi ya hapo. Miaka mingi ilipita na paa la kivuli hiki likawa hatarini kuanguka.
Familia yangu, ikizingatia mazingira ya ibada katika kundi hili na mbaraka aliotukrimia BWANA iliomba ukubali wa kanisa mahalia la Makongo Juu na washiriki waliojisikia kushiriki,tuongoze na kufadhili ujenzi wa banda lile kuwa kanisa. Tarehe 2012 familia yangu na vijana wa SDA Makongo Juu, waliojazwa roho ya Mu
ngu, tuliondoka kwenda kukambika na kuifanya kazi hii. 

Wengi waliokwenda walipanga kushiriki siku chache na kurudi kwenye shughuli zao mjini Dar Es Salaam, lakini roho wa Mungu aliwahimiza kukaa hadi mwisho. Ndani ya siku kumi jengo lilikamilika na kuvunja kambi.

Ni kanisa linaloweza kuchukua watu 200 wakiwa wameketi. Kanisa lina chumba maalum ambacho kinaweza kutumika kama zahanati, huduma muhimu kwa wakazi wa Nyamato, Mkuranga.


Suguti Mission Site, Nyambui

Kanisa la Suguti Mission lililojengwa mwaka 1963 lilikuwa likipokea nusu ya waabudu ndani ya kanisa na nusu ya pili nje kwenye nyasi na magogo ya miti kila sabato kwa muda mrefu. Kutokana na hali hii pia ni wengi walikwisha kukata tamaa ya kuweza kupata viti, na hivi kuacha kufika kwenye ibada.

Pia kanisa hili lilikuwa limeingiliwa na mchwa uliotishia kuangusha ukuta uliokuwa nyuma ya mimbari. Kwa kuliona hili washiriki waliazimia kulifanyia ukarabati kanisa hili. Pia waliweka mikakati ya kujenga kanisa jipya hapo kwenye viwanja vya kanisa hili. Nikiwa kwenye likizo hapa kijijini nilipata taarifa hii kwenye ibada sabato moja. Lakini taarifa ya maandalizi ilikuwa hafifu sana.

 Washiriki walidhani wangefanya ukarabati kwa shillingi takribani millioni moja tu, sawasawa na uwezo wao sio gharama halisi za kazi hii. Pia walianza kuchangia ujenzi wa kanisa jipya na kubwa la Suguti Mission. Tathmini ilionyesha ya kuwa michango ya hali na mali kanisani kukidhi mahitaji ya mikakati hii ilikuwa kidogo kwamba yote miwili isingefanikiwa. Ndipo familia yangu ilipoamua kufadhili mkakati wa ukarabat ikiwemo na upanuzi wa kukidhi hali ya muda mfupi. Kwa muda mrefu ulihitaji kanisa jipya na kubwa zaidi kujengwa.

 Hivi kwa kushirikiana na washiriki wa kanisa la Suguti Mission, wanawake kwa wanaume na watoto, tulilifanyia ukarabati kanisa hili na kuliongeza ukubwa kwa mita za mraba takribani 40. Wale waliokuwa wakiketi nje ya kanisa wakati wa ibada za sabato waliweza kupata nafasi ndani ukarabati ulipokamilika mwaka 2012, lakini waliokwisha kukata tamaa waliendelea kukaa nyumbani kwao, ikiashiria kuteleza na kurudi nyuma katika imani.

Sasa kanisa la Suguti Mission linamwonekano mpya na lenye mvuto kuiko kabla ya hapo. Mimbari imeongezwa ukubwa na hata kwaya zinaweza kuhudumu hapo. Washiriki wana mkakati wa kujenga ule msingi siku za usoni na hili lililopo liwe kanisa la watoto ambao pia ni wengi kama watu wazima.

Kwikonero Site

Kwa kuhisi ya kuwa watu walio wengi waliopenda kufika katika ibada hawafiki, washiriki waliamua kujenga msingi tu wa kanisa jipya la Suguti Mission hapo nyambui kwanza na kuelekeza nguvu zao kwa kanisa jipya huko Kwikonero. Yaani, kujenga kanisa la pili mbali kidogo na lile la kwanza, pembezoni mwa kijiji, kukidhi mahitaji ya walioishi mbali na Mission. Mikakati hii ilikuwa nyeti kwa kazi ya Bwana katika kijiji cha Suguti lakini uwezo wa washiriki ulikuwa ni mdogo.

Familia yangu ilitoa ardhi ya ukoo, ufadhili kwa vile gharama za ujenzi ulikuwa nje ya uwezo wao, na utaalamu wa usanifu na usimamizi wa ujenzi wa mara kwa mara. Kazi ya ujenzi ilianza Novemba 2013 na tarehe 6 Agosti 2014 kanisa lilifunguliwa kwa ibada.

Washiriki walikuwa sahihi kuwaleta waishio mbali katika ibada za sabato kwa njia hii. Sabato hii ya kwanza katika kanisa jipya la Kwikonero liliihudhuriwa na watu 564 kwenye ibada, ikiwa ni zaidi ya uwezo wa makanisa yote mawili yaani la 1963 lililokarabatiwa na kupanuliwa 2012 na hili jipya la 2014. Mwezi mmoja kabla ya ufunguzi huu walibatizwa watu 42 na siku ya ufunguzi darasa la ubatizo lilikuwa na wanafunzi zaidi ya 50 wapya wakitafuta kumjua Yesu Kristo na msalaba wake wa ajabu.

Mungu wetu wa mbinguni ametufunulia na kutufundisha uwezo uliopo katikati ya washiriki wakifanya kazi ya Mungu kwa pamoja na kwa upendo na vile vile umuhimu wa kuwa na nyumba za ibada zenye kukidhi mahitaji ya: idadi kubwa ya watu wanaovutwa kwa Kristo siku kwa siku, ukaribu wa makanisa kwa watu wasiokuwa na njia za usafiri zaidi ya miguu yao, na makanisa yaliyojengwa kwa viwango vya juu kadri ya kuvuta hata roho zenye kusitasita.

Kanisa hili jipya la 2012 ni la kiwango cha juu sana linalovuta mijadala kwa wapita njia ya kuwa “wa-SDA hawana uwezo wa kujenga makanisa kama haya vijijini”. Yaani kumbe wa-SDA wameonekana kuwa wakristo wasiojali ni wapi wanamwabudu Mungu – watu wenye vipaumbele visivyo heshimu utukufu wa Mungu mithili ya wana wa Israeli wakati wa nabii Hagai (Hagai 2).